Wednesday, October 9, 2019

NAIBU WAZIRI DKT MABULA: HALMASHAURI ZIPITIE UPYA MAENEO YALIYOTENGWA KWA SHUGHULI ZA KIJAMII

Halmashauri zote nchini zimetakiwa kupitia upya maeneo yaliyokuwa yametengwa kwaajili ya shughuli mbalimbali za kijamii kama vile makaburi, maeneo ya wazi, ujenzi wa taasisi za umma na masoko ili kujiridhisha kama yanafaa kutumika kwa kusudio la awali au la ili kuyarasimisha kwa wananchi baada ya Serikali kupokea malalamiko ya wananchi kushindwa kurasimishiwa na halmashauri.

Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula wakati akikagua utekelezaji wa zoezi la ukaguzi wa maeneo yaliyovamiwa kwa wilaya za Ilemela na Nyamagana zenye jumla ya maeneo 40, linalotekelezwa na wataalamu wa Wizara ya ardhi, ofisi za ardhi kanda ya Ziwa na maafisa ardhi wa wilaya hizo ambapo amekemea kitendo kinachofanywa na baadhi ya halmashauri nchini cha kutolipa fidia katika maeneo wanayoyatwaa kunakopelekea kuzalisha migogoro isiyo ya lazima na uvamizi mpya katika maeneo hayo

‘..  Halmashauri zote nchini naziagiza kupitia upya maeneo yaliyokuwa yametengwa kwa shughuli za kijamii ili tujue maeneo hayo yamevamiwa kwa kiasi gani tuwafanyie urasimishaji wananchi walipe kodi ya Serikali na kama eneo bado halijavamiwa basi tulilinde ili liendelee kutumika kwa matumizi yaliyokusudiwa ..’ Alisema

Aidha Naibu Waziri  Dkt Mabula amewataka wataalamu wa ardhi nchini kuacha kukaa ofisi badala yake waende kwa wananchi ili kuepuka kuitia hasara Serikali kwa kutoa taarifa zisizo na uhakika huku akiwatoa hofu wananchi wa mitaa ya Nyagungulu, Mwambani na Bukengwa  kata ya Ilemela kuwa Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli ni sikivu itaendelea kutatua migogoro ya ardhi kwa kuzingatia haki, sheria na ubinadamu.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Mhe Stanslaus Mabula mbali na kumpongeza Naibu Waziri huyo kwa kazi kubwa anayoifanya,  Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Magufuli kwa kuunda timu ya mawaziri kupita maeneo yote yenye changamoto za ardhi huku akiiomba halmashauri ya jiji la Mwanza kuharakisha ulipaji wa fidia kwa wananchi wenye migogoro ya ardhi.

Akihitimisha Kamishina wa Ardhi Kanda ya Ziwa Ndugu Mkwasa Buswalo amefafanua kuwa zoezi la ukaguzi wa maeneo yaliyokuwa yametengwa kwa shughuli za kijamii lilianza Septemba 30, 2019 na kumalizika Oktoba 04, 2019 kabla ya kuongezwa siku nne na Naibu Waziri huyo, Sambamba na kuomba ushirikiano kutoka kwa wananchi na viongozi ili kukamilisha zoezi hilo kwa uharaka na ufanisi zaidi.



















No comments:

Post a Comment