Saturday, October 12, 2019

DKT MABULA: VITAMBULISHO VYA KURA VYA NEC HAVITATUMIKA UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

Vitambulisho vya kupiga kura vilivyotolewa  na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) havitatumika katika zoezi la uchaguzi wa Serikali za mitaa unaosimamiwa na Wizara ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI)

Kauli hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati akishiriki zoezi la uandikishaji wa daftari la wapiga kura katika uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwezi Novemba mwaka huu katika kata ya Kirumba wilaya ya Ilemela ambapo amewataka wananchi wa jimbo hilo kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ili wapate fursa ya kuchagua viongozi wenye uwezo, watenda haki, wasimamia maendeleo, wenye hofu na Mungu na watakaoweza kwenda sambamba na kasi ya Rais Mhe Dkt John Magufuli ya kuwaletea wananchi maendeleo

‘.. Kumekuwa na watu wasio na nia njema wanapita katika majumba ya watu wanapotosha, Wanauliza kama una kile kitambulisho cha mpiga kura cha zamani kile cha NEC, Ukisema unacho wanasema basi wewe hauhitaji kujiandikisha wanasahu kuwa uchaguzi huu hatutatumia vitambulisho hivyo  ..’ Alisema

Aidha Mbunge huyo amekemea kitendo hicho kwa kuwa kinakinzana na utaratibu wa uchaguzi wa Serikali za mitaa kuwa mtu yeyote ambae hakujiandikisha katika daftari la mpiga kura hatakuwa na sifa ya kupiga kura.

Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Ilemela, Afisa tarafa wa wilaya hiyo  Ndugu Godfrey Mnzava amesema kuwa Serikali haitavumilia chama chochote cha siasa au kiongozi wake atakaeshiriki kukwamisha zoezi la uandikishaji na hata uchaguzi wenyewe wa Serikali za mitaa huku akiwataka wananchi wa wilaya hiyo kutoa taarifa katika vyombo vya dola juu ya watu wenye nia hiyo ovu.

Akihitimisha afisa mwandikishaji wa daftari la mpiga kura katika mtaa wa Kirumba kati Ndugu Abraham Kapama amesema kuwa bado kuna muitikio hafifu kwa wananchi wa mtaa huo kujitokeza kujiandikisha kwani mpaka sasa idadi ya watu waliojiandikisha ni 111 ingawa jitihada zinachukuliwa kwa kupita mitaani kutangaza na kupiga pembe ili wananchi waweze kujitokeza kwa wingi ukilinganisha na wale waliojitokeza katika zoezi la BVR.

' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga '

Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
Oktoba 12, 2019.








No comments:

Post a Comment