Saturday, October 12, 2019

KIVUKO CHA KISIWA CHA BEZI CHAKAMILIKA KWA 85%

Kivuko kilichogharimu zaidi ya Bilioni 2.7 kinachojengwa na kampuni ya Songoro Marine ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa wananchi wa kata ya Kayenze kimefika 85% ya ujenzi wake ambapo mapema mwezi Novemba mwaka huu kinategemewa kuanza majaribio katika Ziwa Viktoria ili kiweze kutumika na wananchi.

Hayo yamebainika wakati wa ziara ya mbunge wa Jimbo hilo katika Kisiwa cha Bezi kata ya Kayenze ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za mara kwa mara anazozifanya kwa wananchi wake ili kuwasikiliza changamoto zao, kuzipatia ufumbuzi na kuhamasisha maendeleo ambapo amesema anaridhishwa na kasi ya ujenzi wa Kivuko hicho kitakachochukua watu wenye uzito wa tani zaidi ya 250 na magari 10

‘.. Kivuko hiki nia ahadi tuliyoitoa kipindi tunaomba ridhaa kwa wananchi wa Kayenze, Na wakati tunaitoa hatukuwa na uhakika sana kwasababu haikuwa katika utaratbu uliopangwa wa namna hii, bahati nzuri tulipoingia tukapeleka wazo kwa wizara husika na wizara ikapeleka kwa mheshimiwa Rais na leo kama mnavyoona zaidi ya 85% imekamilika ..’ Amesema

Aidha Mbunge huyo ameishukuru Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli kwa namna inavyojali wananchi wake  huku akiwaasa wananchi wa Kisiwa hicho kuongeza kasi ya uzalishaji ili kuleta tija na maana ya kuja kwa usafiri huo utakaosaidia kuongeza thamani za biashara wanazozifanya hasa za samaki na mazao yake ili kuinua uchumi wao.

Akimkaribisha mbunge huyo, Afisa Tarafa wa wilaya ya Ilemela Bwana Godfrey Mnzava amekemea vitendo vya uvunjifu wa amani vinavyoanza kujitokeza kisiwani humo kwa baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi sambamba na kuwataka viongozi wa Serikali za mtaa huo kuitisha vikao vya kisheria kikiwemo kile cha uwasilishaji wa taarifa za mapato na matumizi kwa wananchi 

Kwa upande wake Bi Neema Dioniz akiwakilisha wananchi wenzake wa Mtaa wa Kisiwa cha Bezi wameishukuru Serikali na mbunge wao kwa kuwasaidia upatikanaji wa usafiri huo huku akiahidi kukitunza na kukitumia katika kujiongezea kipato

Ziara hiyo ilihudhuriwa na wataalamu kutoka manispaa ya Ilemela na viongozi wa chama cha mapinduzi wilaya ya Ilemela wakiongozwa na katibu wa CCM wa wilaya hiyo Comred Michael Chonya ambae amethibitisha kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi wa chama chake chini ya mbunge na Rais Dkt John Magufuli.

' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga '

Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
Oktoba 11, 2019.











No comments:

Post a Comment