Monday, October 14, 2019

MBUNGE ILEMELA AHITIMISHA MASHINDANO YA MAGA MCHANGANI NDONDO CUP IGOMBE.

Mashindano ya Maga Mchangani Ndondo Cup yaliyohusisha Timu 12 kutoka maeneo ya Igombe na viunga vya jirani yamehitimishwa na mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa kukabidhi zawadi kwa Timu zilizoshinda na kuzungumza na hadhara iliyohudhuria mashindano hayo.

Akizungumza na hadhara hiyo Mhe Dkt Angeline Mabula mbali na kumpongeza muandaaji wa mashindano hayo, Amewataka vijana wa Igombe na jimbo la Ilemela kwa ujumla kutumia fursa za uwepo wa mashindano mbalimbali  ndani ya jimbo hilo kuibua vipaji vyao na kuviendeleza, kujenga undugu na mshikamano, kujenga nidhamu, kujiburudisha na kuifanya michezo kuwa ajira ili kujikwamua kiuchumi 

‘.. Niwapongeze kwa mashindano haya ya Ndondo Cup ya mchangani, Ukiweza kucheza hapa na ukashinda kwa vyovyote vile stamina ukipelekwa kwenye uwanja wa kawaida basi wewe si mtu wa kawaida ..’ Alisema

Aidha Mhe Dkt Mabula alikabidhi Kuku mmoja kwa mshindi wa tatu ambae ni Timu ya Warriors, kuku wawili kwa mshindi wa pili ambae ni Timu ya The Best na Mbuzi mmoja kwa mshindi wa kwanza ambae ni Timu ya Kings, huku akiahidi kuchangia zawadi ya Ng’ombe kwa mshindi wa kwanza, Mbuzi wawili kwa mshindi wa pili na mbuzi mmoja kwa mshindi wa tatu utakapoanza msimu wa tatu wa mashindano hayo unaotarajiwa kuanza baada ya wiki 2 tangu kumalizika kwa msimu huu wa pili.

Katika hatua nyingine,  Mhe Dkt Angeline Mabula amefanya ziara katika mtaa wa Kabangaja kata ya Bugogwa kwa kusikiliza kero za wananchi, kuhamasisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo ambapo amemshukuru Rais Mhe Dkt John Magufuli kwa utekelezaji wa miradi ya kimkakati ndani ya jimbo lake, sanjari na kutatua kero ya maji ya muda mrefu iliyokuwa ikiwakabili wananchi hao kwa kukabidhi mabomba ili waunganishiwe maji kuanzia siku ya Jumanne ya Oktoba 15, 2019.






No comments:

Post a Comment