Monday, October 14, 2019

RC MWANZA ARIDHISHWA NA KASI YA SEKTA YA MICHEZO ILEMELA.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe John Mongela ameridhishwa na kasi ya ukuaji wa sekta ya Michezo katika halmashauri ya manispaa ya Ilemela hivyo kuzitaka halmashauri nyingine za mkoa huo kujifunza kutoka katika wilaya hiyo.

Rai hiyo ameitoa wakati akizindua viwanja vya Michezo vya kisasa vilivyojengwa katika shule ya msingi Sabasaba kata ya Ilemela kwa ufadhili wa wadau wa michezo wa Sport Charity vilivyojumuisha mchezo wa mpira wa miguu, mpira wa pete, mpira wa mikono, mpira kikapu, mpira wa wavu, eneo la kupumzikia mashabiki na jengo la kutunzia vifaa na kubadilishia nguo ambapo amesifu manispaa hiyo na viongozi wake akiwemo Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa namna wanavyopambana kuhakikisha wilaya hiyo inaongoza katika kuimarisha sekta hiyo

‘.. Lazima niseme Mimi nna halmashauri nane katika mkoa wangu, Lakini hata nikienda halmashauri zingine nakutana na walimu wa Michezo wa kutoka Ilemela ndio wanachangamsha halmashauri hizo, Nisionekane napendelea nataka kusema wanatusaidia sana na nawapongeza..’ Alisema

Aidha Mhe Mongella mbali na kuishukuru CCM kwa kutoa eneo la ujenzi wa kiwanja hicho, ameiasa manispaa ya Ilemela kukitunza na kuanza kukijengea uzio ili kukilinda huku akiahidi mifuko mia moja ya Saruji kwaajili ya ujenzi wa uzio wa kiwanja.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula ameishukuru taasisi ya Sport Charity kwa mradi huo huku akiwaomba wadau wengine kujitokeza ili kuboresha sekta hiyo ya michezo ndani ya jimbo lake sambamba na kusisitiza wananchi kujitokeza kukitumia kiwanja hicho.

Nae katibu wa Taasisi ya Sport Charity Ndugu Isack Mwanahapa amesema kuwa ujenzi wa kiwanja hicho ulianza Oktoba, 2018 huku akimshukuru mbunge wa jimbo la Ilemela kupitia taasisi yake ya The Angeline Foundation kwa msaada wa matofali 1100 yaliyotumika katika kukamilisha kiwanja hicho na Kampuni ya Kichina ya Sinohydro kwa kutoa vifaa vya kusawazisha.

Akihitimisha kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Ilemela, Afisa Tarafa wa Ilemela Ndugu Godfrey Mnzava amewataka wafanya biashara waliokuwa wakitumia kiwanja hicho kwaajili ya biashara za mnada kuacha kuchimba ndani ya kiwanja hicho huku akiwaomba kutumia eneo mbadala walilokuwa wametengewa hapo awali kwa biashara zao.





















No comments:

Post a Comment