Saturday, February 8, 2020

CCM YARIDHISHWA NA UTEKELEZAJI WA ILANI ILEMELA.

Chama Cha Mapinduzi wilaya ya Ilemela kimeridhishwa na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015-2020 uliofanywa ndani ya wilaya hiyo katika miradi mbalimbali ikiwemo ya afya, miundombinu, elimu, maendeleo ya jamii, kilimo, maji, ardhi na mipango miji.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Ilemela Mhe Nelson Mesha wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo  iliyotekelezwa ndani ya wilaya hiyo katika kipindi cha Serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe Rais Dkt John Magufuli kupitia Ilani ya uchaguzi na ahadi zake alizozitoa  kwa wananchi wa wilaya hiyo ambapo ameipongeza manispaa ya Ilemela na viongozi wake kwa uadilifu, usimamizi mzuri na ufuatiliaji wa miradi yake  huku akiwataka kulipa fidia za maeneo wanayoyatwaa kwa wananchi, kuanza kufikiria ujenzi wa majengo ya ghorofa na ujenzi wa uzio kwa miradi yenye uhitaji wa kufanya hivyo ili kuilinda dhidi ya uhalifu unaoweza kujitokeza

'.. Nawapongeza sana kwa kazi kubwa mnayoifanya, mkurugenzi na timu yako mmefanya kazi kubwa sana ingawa siwezi kusema muwe wa kina nani kwa kazi hii nzuri mliyoifanya ..' Alisema

Katibu wa CCM wilaya ya Ilemela Bi Aziza Juma Isimbula akafafanua kuwa ziara hiyo ya ukaguzi wa miradi ni moja wapo ya njia za uadhimishaji wa sherehe za kuzaliwa kwa chama hicho na kufikia miaka 43 tangu kuanzisha kwake hivyo kuwataka wananchi kuendelea kukiamini na kukiunga mkono.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Dkt Severine Mathias  Lalila kama muwakilishi wa Chama ndani ya Serikali ya wilaya amewahakikishia ushirikiano viongozi hao  katika kuhakikisha yaliyoahidiwa na Mhe Rais yanatekelezwa na kutimia kwa wakati huku Mstahiki Meya wa manispaa ya Ilemela Mhe Renatus Mulunga akisema kuwa baraza lake la madiwani litaendelea kuisimamia manispaa na watendaji wake kuhakikisha wananchi wake wanaendelea kupata maendeleo.

Nae mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Ndugu John Paul Wanga mbali na kumshukuru Mhe Rais na Mbunge wa Jimbo hilo Mhe Dkt Angeline Mabula kwa msukumo wake wa kufuatilia utekelezaji wa miradi na kutoa matofali yote yanayotumika katika ukamilishaji wa miradi ya elimu, afya na baadhi ya ofisi za Serikali za mitaa na chama tawala kwa fedha za mfuko wa Jimbo na ushawishi binafsi kwa wadau kupitia taasisi yake ya The Angeline Foundation, huku akiongeza kuwa shilingi bilioni 4 zitatumika katika kukamilisha ujenzi wa barabara ya Nyakato kuelekea Buswelu na fidia ya nyumba mbili zilizoathirika na mradi huo italipwa na manispaa yake na mradi wa maji Nyasaka ukigharimu kiasi cha Euro Milioni 2.1 unaotekelezwa chini ya mkandarasi kampuni ya kizalendo ya JR Construction wakati mradi wa kituo cha afya Buzuruga wenye jengo la huduma za mama na mtoto, jengo la kuhifadhia maiti, jengo la kufulia,jengo la wagonjwa wa nje, jengo la maabara, nyumba ya mtumishi, njia ya kutembelea,  ukigharimu shilingi milioni 400 kutoka Serikali kuu sanjari na kuahidi ujenzi wa duka la dawa la kisasa litakalojengwa kwa mapato ya ndani ya manispaa hiyo mapema mwaka huu wa fedha.

Ikumbukwe kuwa utekelezaji wa miradi ya Maendeleo katika Jimbo la Ilemela ni matokeo ya Sera ya Utatu kwa maana ya wananchi kuanzishwa misingi ya miradi husika, Mbunge Dkt Angeline Mabula anatoa matofali yote yatakayohitajika katika mradi husika kupitia fedha za mfuko wa Jimbo na Taasisi yake ya The Angeline Foundation na kisha manispaaa hubeba jukumu la umaliziaji wa miradi hiyo.













No comments:

Post a Comment