Sunday, March 8, 2020

WIZARA YA AFYA YAMTEUA DKT MABULA KUWA BALOZI WA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA MWANZA.

Wizara ya afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kitengo kikuu cha maendeleo ya jamii kupitia msafara wake wa matembezi ya kutokomeza ukatili wa kijinsia umemteua mbunge wa jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kuwa balozi wa kupinga ukatili wa kijinsia  katika mkoa wa Mwanza.

Akizungumza wakati wa sherehe za kuelekea kilele cha siku ya wanawake duniani zilizofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Bugogwa wilaya ya Ilemela na kupambwa na kauli mbiu ya KIZAZI CHA USAWA KWA MAENDELEO YA TANZANIA YA SASA NA BAADAE kiongozi wa msafara wa kutokomeza ukatili wa kijinsia chini ya wizara hiyo, Bi Hanifa Selengu amesema kuwa msafara wake umekuwa ukipitia mikoani na wilayani kuhamasisha  wananchi juu ya kupiga vita dhidi ya unyanyasaji, ukatili wa kijinsia na watoto na kutoa huduma mbalimbali kwa jamii ikiwemo msaada wa kisheria bure, na elimu ya afya kwa wananchi wa maeneo husika na katika mkoa wa Mwanza wamebahatika kutembelea wilaya za Misungwi na Ilemela wakishirikiana na wadau kutoka taasisi binafsi za chama cha wanasheria wanawake TAWLA, TAHEA, WE EFFECT na Mwanza Rural Housing hivyo kutokana na kuridhishwa na kujitoa na kuunga mkono mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, upigaji vita wa unyanyasaji na mapambano dhidi ya  ukandamizaji wa umiliki wa ardhi unaofanywa na mwanamama mbunge wa jimbo la Ilemela ambae pia ndie naibu waziri wa wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Mhe Dkt Angeline Mabula msafara wake umeamua kumteua kuwa balozi wa kupinga ukatili wa kijinsia na kumuomba kukubali na kuendelea na juhudi zake hizo ili kuisaidia jamii kutokomeza kabisa hali hiyo

' Kupitia hadhara hii tumemteua mbunge wenu mwanamama Mhe Dkt Angeline Mabula kuwa balozi wa kupinga ukatili katika mkoa wa Mwanza na tulivyopeleka jina kwenu na kufanya udadisi dhidi yake bahati nzuri kila moja alikubali ' Alisema

Aidha kiongozi huyo wa msafara wa matembezi ya kutokomeza ukatili wa kijinsia unaoelekea mkoani Simiyu kwenye kilele cha sherehe za maadhimisho ya siku ya wanawake duniani ambayo hufanyika kila Machi 08, alitumia pia hadhara hiyo kumtangaza mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Dkt Mathias Severine Lalika kuwa balozi wa kupinga ukatili wa watoto kutokana na juhudi zake za kupinga mimba za utotoni mashuleni na kuwaomba wananchi kuendelea kuwaunga mkono viongozi hao.

Kwa upande wake Mhe Dkt Angeline Mabula mbali na kushukuru kwa uteuzi huo ameipongeza Serikali na Rais Mhe Dkt John Magufuli kwa kuendelea kuwaamini wanawake na kuwateua kushika nafasi mbalimbali za uongozi huku akiwaomba wanawake wengine kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu sanjari na kufafanua hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali kupitia wizara anayohudumu ya Ardhi katika kusaidia wanawake ikiwemo suala la usawa katika kumiliki ardhi na kupambana na migogoro ya ardhi ambayo kwa kiasi kikubwa imepungua.

Nae mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe  Dkt Mathias Lalika ameushukuru msafara huo kwa kupita katika wilaya yake sanjari na kueleza chanzo cha kuwepo kwa siku hiyo baada ya kufanyika kwa mkutano wa Beijing wa mwaka 1995 hivyo kuwataka wanawake kuitumia siku hiyo kwaajili ya kuzipatia ufumbuzi kero na changamoto zinazowakabili.










No comments:

Post a Comment