Monday, October 27, 2025

CCM KUFUNGA KAMPENI KWA KISHINDO MWANZA, DKT SAMIA AWEKA REKODI YA WATU MILIONI 25

 Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi, amewaomba wakazi wa Mwanza na maeneo jirani kujitokeza kwa wingi katika mkutano wa kufunga kampeni za chama hicho utakaofanyika kesho, Oktoba 28, 2025, katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.


Akizungumza leo, Oktoba 27, 2025, katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) jijini humo, Kihongosi amesema mkutano huo utakuwa wa kihistoria na utadhihirisha ukubwa, uimara na umadhubuti wa Chama Cha Mapinduzi nchini.

Ameeleza kuwa kufikia leo, mikutano ya kampeni ya Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka rekodi ya kipekee baada ya kuhudhuriwa na watu zaidi ya milioni 25.3 katika mikutano zaidi ya 114 iliyofanyika nchi nzima.

Kihongosi amesema idadi ya watu waliokuwa wakifuatilia mikutano hiyo kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii imefikia milioni 57.1, huku takwimu za kimtandao zikionesha kuwa Dkt. Samia amefuatiliwa mara milioni 164.9 — idadi ambayo haijawahi kushuhudiwa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini.

Amebainisha kuwa takwimu hizo zinaonyesha ukubwa wa ushawishi wa Dkt. Samia na kukubalika kwake kwa wananchi kutokana na kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wake. Aidha, amesema mafanikio ya kampeni hizo ni kielelezo cha nguvu ya chama hicho na mwitikio chanya wa wananchi kwa sera na utekelezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita.


No comments:

Post a Comment