WACHAMBUZI wa masuala ya siasa, diplomasia na maendeleo wamewataka vijana na wananchi kwa ujumla kutumia mitandao ya kijamii kwa busara, uangalifu na uzalendo, wakisisitiza umuhimu wa kufanya tathmini ya kina kuhusu ukweli wa taarifa wanazopokea na kusambaza, hususan katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu.
Wito
huo umetolewa Oktoba 26, 2025 jijini Dar es Salaam wakati wa mdahalo wa
“Wajibu wa Kidijitali kwa Amani ya Nchi Kabla, Wakati na Baada ya
Uchaguzi” uliofanyika katika ukumbi wa American Corner, Makumbusho ya
Taifa. Mdahalo huo uliandaliwa kwa lengo la kujadili namna teknolojia na
mitandao ya kijamii inaweza kutumika kuimarisha amani, umoja na
mshikamano wa kitaifa katika kipindi nyeti cha uchaguzi.
Akizungumza
katika mjadala huo, mchambuzi wa masuala ya diplomasia na siasa,
Abdulkarim Atik, alisema vijana wanayo nafasi kubwa katika kuamua
mwelekeo wa taifa kupitia mitandao ya kijamii. Alisema ni muhimu
kutathmini ukweli wa taarifa kabla ya kuzisambaza kwa sababu taarifa
zisizo sahihi zimekuwa chanzo cha taharuki, migawanyiko na uhasama
katika jamii.
“Ikiwa
vijana watatambua ukweli wa taarifa wanazopata, itawasaidia kufanya
maamuzi sahihi na kuchangia katika kulinda amani ya nchi, hususan
kipindi cha uchaguzi,” alisema Atik.
“Mara
nyingi propaganda hujificha katika sura ya habari. Tunapaswa kuwa
makini tusitumike kueneza ajenda zinazolenga kugawa taifa.”
Kwa
upande wake, mwandishi wa habari wa Crown Televisheni, Imani Luvanga,
alisema mitandao ya kijamii si adui wa jamii kama wengi wanavyodhani,
bali ni nyenzo muhimu ya mawasiliano, elimu na maendeleo, ikiwa
itatumiwa kwa uangalifu.
“Tatizo
siyo mitandao, bali ni namna watu wanavyoiendesha. Matumizi sahihi
yanaweza kuleta manufaa makubwa, yakiwemo maendeleo ya kiuchumi na
kijamii,” alisema Luvanga.
“Vijana
wanapaswa kujitambua wanapotumia mitandao hiyo—waelewe sababu ya
kuitumia, aina ya taarifa wanazozingatia na faida wanazotarajia kupata.”
Luvanga
alisisitiza kuwa mitandao inaweza kuwa daraja la fursa kwa vijana
wanaojihusisha na ujasiriamali, ubunifu na uandishi wa habari, iwapo
itatumika kwa kujenga badala ya kubomoa. Aliongeza kuwa jamii inapaswa
kujifunza kutumia majukwaa hayo kuhamasisha amani na ushirikiano badala
ya maneno ya chuki.
Mdau
wa siasa na maendeleo, Reeves Ngalemwa, alisisitiza umuhimu wa
kuimarisha misingi ya uzalendo tangu utotoni, akisema ni msingi wa taifa
lenye uthabiti katika zama za kidijitali. Kwa mujibu wake, kuandaa
watoto kuwa wazalendo kunasaidia kizazi kipya kutambua lipi ni sahihi na
lipi si sahihi katika taarifa zinazozunguka mitandaoni.
“Ni
muhimu kuweka mazingira ya kuwaandaa watoto kujifunza uzalendo tangu
wakiwa shule za msingi ili wakue wakiwa na mapenzi ya kweli kwa nchi
yao,” alisema Ngalemwa.
“Tunapojenga
kizazi chenye misingi imara ya uzalendo, tunajenga jamii inayotumia
teknolojia kwa manufaa ya taifa, si kwa uharibifu.”
Kwa
upande wake, mchambuzi wa masuala ya vyombo vya habari na mpiga picha
maarufu, Issa Michuzi, alihimiza wananchi kuwa makini na taarifa
zinazochochea chuki au migawanyiko, akibainisha kuwa propaganda zinaweza
kuathiri umoja wa kitaifa endapo hazitachunguzwa kwa makini.
“Watu
wanatakiwa kuangalia mambo kwa umakini. Propaganda inaweza kuwa nzuri
au mbaya. Tumefika hapa si kwa bahati mbaya, ni matokeo ya kuruka
hatua,” alisema Michuzi.
“Kila
mmoja awe mlinzi wa taifa kwa kutathmini taarifa kabla ya kuzisambaza.
Mitandao inaweza kujenga au kubomoa, inategemea namna tunavyotumia.”
Michuzi
alionya kuwa kutokuwa makini katika kusambaza taarifa zisizo sahihi
mitandaoni kunaweza kusababisha jamii kuingia katika migogoro isiyo ya
lazima, na kusisitiza kuwa kila raia ana wajibu wa kulinda amani kwa
vitendo, ikiwemo nidhamu ya kidijitali.
Mwenyekiti
wa Tanzania Bloggers Network (TBN), Beda Msimbe, aliwataka vijana kuwa
na ndoto zilizoegemea katika muktadha wa kitaifa, akisema maamuzi yao ya
kisiasa na kijamii yanapaswa kuweka mbele maslahi ya taifa. Alisisitiza
umuhimu wa vijana kuwa na mtazamo mpana katika kuchambua matukio na
taarifa wanazokutana nazo.
“Vijana wanahitaji msingi imara ili maamuzi yao yawe ya kusonga mbele badala ya kuumiza taifa,” alisema Msimbe.
“Tunapaswa kuwa na kizazi kinachofikiri kitaifa, si kizazi kinachoendeshwa na matukio ya muda mfupi kwenye mitandao.”
Mdahalo
huo uliokuwa chini ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wachambuzi, Magid
Mjengwa, ulihudhuriwa na wadau mbalimbali wakiwemo wahariri wa
mawasiliano ya kidijitali, wanabloga kutoka TBN, wanafunzi wa Chuo cha
Diplomasia, wadau wa amani na waandishi wa habari.
Washiriki
walikubaliana kuwa mitandao ya kijamii ni uhalisia usioweza kuepukika
katika maisha ya sasa, hivyo ni muhimu kwa Watanzania wote—hasa
vijana—kuijua na kuitumia kwa manufaa ya taifa.
Mdahalo
ulihitimishwa kwa wito wa pamoja wa kuimarisha elimu ya habari (media
literacy) na maadili ya kidijitali, sambamba na kujenga utamaduni wa
kuthamini ukweli na amani.
“Tanzania
ni nchi ya amani. Tunapaswa kuhakikisha mitandao inabaki kuwa chombo
cha kuunganisha Watanzania, si kuwatenganisha,” alihitimisha Mjengwa.





No comments:
Post a Comment