Akizungumza katika mkutano
wa kufunga kampeni uliofanyika katika Viwanja vya Godauni, Kata ya
Mkuranga, Mheshimiwa Ulega aliwataka wananchi waendelee kuiamini kazi
kubwa inayotekelezwa na Serikali chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu
Hassan, akisisitiza kuwa Mkuranga haijawahi kushuhudia kasi ya maendeleo
kama ilivyo sasa.
“Asiyeshukuru
kwa yai, hata jogoo hachinjiwi. Nendeni mkamchague Dkt. Samia Suluhu
Hassan, mkanichague mimi kijana wenu, pamoja na madiwani wetu wa kata
zote za Jimbo la Mkuranga,” alisema Ulega.
Ulega
alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wa
Rais Dkt. Samia, Wilaya ya Mkuranga imepata miradi mikubwa ya maendeleo
kuliko wakati mwingine wowote tangu kuanzishwa kwake, ikiwemo miradi ya
elimu, afya, maji na barabara.
Aidha,
Mgombea huyo wa CCM alitumia mkutano huo kuwahakikishia wananchi kuwa
vyombo vya usalama vimejipanga ipasavyo kuhakikisha uchaguzi mkuu
utafanyika kwa amani, utulivu na haki, bila mwananchi yeyote kudhurika.
“Serikali
haiwezi kuruhusu haki ya wananchi kupiga kura ivurugwe na watu wachache
wanaotumia mitandao ya kijamii kueneza taharuki. Tumewekeza kwa kiwango
kikubwa kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia unaimarishwa,” aliongeza
Ulega.
Ulega
alihitimisha kwa kuwataka wananchi wa Mkuranga kudumisha amani na umoja
wakati wote wa mchakato wa uchaguzi, akisisitiza kuwa maendeleo
yaliyofikiwa ni matokeo ya uongozi bora wa CCM na ushirikiano wa
wananchi.

No comments:
Post a Comment