Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Profesa Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto), akikagua jenereta
linalowezesha mnara wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL), katika eneo la
eneo la Gairo Hill, wilayani Gairo, Mkoani Morogoro. Wa kwanza kulia ni
Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchembe.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewaonya
wananchi kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ya mawasiliano ili
wasingie katika janga la kushughulikiwa na sheria kali inayodhibiti
matumizi hayo mabaya ya mitandao.
Amesema, wakati jitihada
zinaendelea kufanyika kuhakikisha huduma za mawasiliano ya simu kuwa
bora zaidi na pia kuwafikia Watanzania wengi, baadhi wamekuwa wakitumia
mitandao vibaya badala ya kuitumia kwa ajili ya kutafuta maendeleo.
"Wanaotumia
mitandao hii vibaya, pamoja na kupata hasara, lakini ni vema wakaacha
mara moja tabia hiyo vinginevyo watajikuta wameingia katika janga la
kushughulikiwa na sheriaa kali ambazo tayari zipo kwa ajili ya kudhibiti
matumizi hayo mabaya ya Mitandao", alisema prof. Mbarawa.
Pia
amezita kampuni za simu nchini kuhakikisha mawasiliano ya simu
yanapatikana wakati wote katika ubora unaotakiwa ili kuwawezesha
wananchi kupata huduma inayowiana na thamani ya fedha wanayolipa.
Akikagua
na kuzindua minara ya simu ya kampuni za TTCL, VODACOM, HALOTEL, na
TIGO katika Wilaya ya Gairo mkoani Morogoro, Profesa Mbarawa amesema
Serikali itaendelea kushirikiana na kampuni za simu kupitia Mfuko wa
Mawasiliano kwa wote UCSAF ili katika kipindi cha miaka mitatu ijayo
sehemu zote za Tanzania ziwe zimefikiwa na huduma ya mawasiliano ya simu
ya uhakika.
"Tumieni mawasiliano ya simu kufanya biashara,
kuboresha huduma za jamii kama elimu na habari ili kukuza ustawi wa
maisha yenu", amesema Profesa Mbarawa.
Amezungumzia umuhimu wa
kampuni za simu kujenga minara katika maeneo mapya na kukarabati minara
ya zamani ili kuwezesha mawasiliano kuwa katika ubora maeneo yote ya
nchi.
Amewataka wakazi wa vijiji vya Letugunya, Leshata na
Chakwale kutumia fursa ya upatikanaji wa mawasiliano kuongeza uzalishaji
wa mazao na kuyauza kwa bei nzuri na hivyo kukuza uchumi wao.
Kwa
upande wake Mtendaji mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote Mhandisi
Peter Ulanga amemhakikishia Waziri Profesa Mbarawa kuwa mfuko huo
umejipanga kukamilisha miradi yote kwa wakati na kufanya uhakiki wa
takwimu za mawasiliano nchi nzima ili kubaini maeneo ambayo yana
changamoto kubwa ya mawasiliano na kuyatatua.
Mkuu wa Wilaya ya
Gairo Siriel Mchembe amemshukuru Waziri Mbarawa kwa kuboresha huduma za
mawasiliano katika Wilaya hiyo na kumhakikishia wananchi watailinda
miundombinu hiyo ili idumu kwa muda mrefu.
No comments:
Post a Comment