Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na
Mipango Amina Khamis Shaaban na Naibu Mkuu wa Ushirikiano wa kiuchumi
Kanda ya Afrika Mashariki kutoka Ujerumani Georg Rademacher,
wakibadilishana kumbukumbu za Mkutano wa Mashauriano baada ya
kusazisaini katika Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dar es
Salaam, leo.
NA MWANDISHI MAALUM, DAR ES SALAAM
Ujerumani
imeipatia Tanzania kiasi cha Euro milioni 198.5 sawa na Sh. Bilioni
520.86 zilizotumika kufadhili miradi mbalimbali ikiwemo ya Maliasili na
Mazingira, Afya, Maji, Nishati, Udhibiti wa Fedha za Umma (Good
Financial Governance) na Kusaidia Huduma za Wakimbizi katika mkoa wa
Kigoma, katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.
Hayo
yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha
na Mipango, Bi. Amina Khamis Shaaban wakati wa tukio la Tanzania na
Ujerumani kusaini kumbukumbu za Mkutano wa Mashauriano ya Kimaendeleo
(Bilateral Development Consultations) ambapo Ujerumani imeonesha nia ya
kuendelea kuisaidia Tanzania katika Sekta hizo kuanzia mwaka 2018 hadi
2021.
Kumbukumbu
za Mashauriano hayo zimesainiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha
na Mipango Bi. Amina Khamis Shaaban kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania na Naibu Mkuu wa Idara ya Kanda ya Afrika
Mashariki katika Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo ya
Ujerumani Bw. Georg Rademacher kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani.
Mkutano
huo ni maandalizi ya mkutano wa Majadiliano ya Kimaendeleo (Bilateral
Negotiations) kati ya nchi hizi mbili unaotarajiwa kufanyika mwaka 2018
ambapo Serikali ya Ujerumani itatangaza kiasi cha fedha watakazotoa kama
msaada kwa ajili ya kufadhili Sekta zilizoainishwa katika kumbukumbu
zilizosainiwa.
“
Tunaishukuru Ujerumani kwa kuwa miongoni mwa washirika wa muda mrefu
wanaotoa misaada mikubwa ya kimaendeleo kwa Tanzania na sisi tunaahidi
kuendeleza ushirikiano huo kwa faida ya pande zote mbili” alisema Bi.
Amina Khamis Shaaban.
Kwa
upande wake Bw. Georg Rademacher kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani
amesema kwamba Tanzania imekuwa na sifa njema nchini Ujerumani hasa kwa
sababu ya amani iliyopo, jinsi ambavyo imehifadhi maliasili zake na
kuifanya kuwa nchi yenye vivutio vya kipekee vya utalii.
Bwana
Rademacher aliongeza kwamba kwa sasa nchi ya Tanzania imepiga hatua
kubwa sana katika kupambana na ubadhirifu wa mali za Umma na kwamba
Ujerumani itaendelea kuisaidia Tanzania ili kuweza kuleta maendeleo kwa
watu wake na kuondoa umaskini.
No comments:
Post a Comment