Mbunge wa Jimbo la Ilemela na Naibu Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline S.L Mabula amewahakikishia ushirikiano wadau wa maendeleo kutoka nchini Kanada katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni kwake.
Hayo ameyasema leo wakati akizungumza na wadau hao waliofika ofisi za halmashauri ya manispaa ya Ilemela kuzungumza na viongozi wa halmashauri ya manispaa hiyo juu ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo ujenzi wa zahanati ya Lukobe iliyopo jimboni humo sambamba na kuwashukuru kwa kuchagua mtaa wa Lukobe, Ilemela kuwa sehemu ya utekelezaji wa mradi huo.
‘.. Kitu pekee ninachoweza kuwahakikishia ni utayari na ushirikiano wangu, Mimi naamini jamii ikishirikiana na wadau mbalimbali inakuwa rahisi kutekeleza shughuli za kimaendeleo…’ Alisema
Mhe Dkt Angeline Mabula ameongeza kuwa jamii inapaswa kuunga mkono jitihada zote za utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na wadau hao kwa kujitolea nguvu ili kusaidia kukamilika haraka kwa miradi hiyo.
Kwa upande wake kiongozi wa msafara huo ndugu Fred Schaller mbali na kuwashukuru viongozi hao amesema kuwa wameguswa na changamoto zinazokabili wananchi wa jimbo hilo na kuamua kushirikiana na uongozi wa manispaa hiyo kujenga zahanati mtaa wa Lukobe kama mwanzo wa ushirikiano wao katika kumaliza changamoto hizo.
Akihitimisha mkurugenzi wa halmashauri ya manispaa ya Ilemela ndugu John Wanga amesema kuwa manispaa yake itaendelea kuunga mkono jitihada zote za kuhakikisha wananchi wake wanapata maendeleo kwa kuunga mkono wadau wa maendeleo wanaofika wilayani humo kutekeleza miradi mbalimbali.
Ikumbukwe kuwa Jimbo la Ilemela limekuwa likitekeleza shughuli zake za maendeleo kwa Sera ya utatu kwa maana ya kushirikisha nguvu za mbunge wa jimbo, nguvu za mkurugenzi wa manispaa na nguvu za wananchi katika kufanikisha miradi ya maendeleo iliyosaidia kukamilika kwa madarasa 28 na zahanati 4 mpaka sasa.
' Ilemele ni yetu, tushirikiane kuijenga '
Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
21.04.2018
No comments:
Post a Comment