Mashindano ya Angeline Jimbo Cup 2018 yamezidi kutimua
vumbi ambapo kwa siku ya leo yamezikutanisha Timu ya Kata ya Kirumba na
Timu ya Kata ya Nyakato ikiwa ni hatua ya nusu fainali, mechi
iliyochezwa katika uwanja wa Sabasaba kata ya Ilemela.
Katika mchezo huo Timu ya Kata ya Kirumba imefanikiwa
kufuzu kuingia hatua ya fainali ya mashindano hayo mara baada ya
kuinyuka Timu ya Kata ya Nyakato goli moja kwa sifuri, Goli lililofungwa
na mchezaji Baraka David mwenye jezi nambari sita dakika ya 66 ya
kipindi cha pili.
Akizungumza mara baada ya kuisha kwa mchezo huo, Diwani wa
Kata ya Kirumba Mhe Alex Ngusa ameipongeza timu yake kwa ushindi
ilioupata huku akiwaasa wananchi wa kata hiyo na mashabiki wote
kuhakikisha wanaendelea kuunga mkono timu yao ili iweze kuchukua kombe
hilo
‘.. Tumefika nusu fainali tunaelekea hatua ya fainali sasa
na ni umoja, ushirikiano na upendo wa wana Kirumba ndo umetufikisha
hapa, Kwa hiyo naomba nitoe wito kwa wana Kirumba waendelee kuiunga
mkono timu yao …’ Alisema
Kwa upande wake msemaji wa Timu ya Kata ya Nyakato ambae
pia ni Katibu wa uhamasishaji na chipukizi wa UVCCM wa kata hiyo, Ndugu
Edwin Simon amelalamikia Timu pinzani kwa kukiuka sheria na taratibu za
mashindano inayokataza kushirikisha wachezaji wanaocheza ligi kuu na
wachezaji wasiotoka maeneo husika huku akiomba kuchukuliwa hatua kwa
Timu ya Kata ya Kirumba kwa kukiuka utaratibu huo.
Aidha katika mchezo huo, Mchezaji Selemani Hamisi jezi
nambari Tano anaechezea Timu ya Kata ya Kirumba alipewa Kadi Nyekundu
mara baada ya kumchezea rafu mshambuliaji wa Timu ya Kata ya Nyakato.
Mashindano ya Angeline Jimbo Cup 2018 yataendelea tena hapo
kesho saa 2.00 asubuhi katika uwanja wa Sabasaba kata ya Ilemela kwa
kuzikutanisha timu ya kata ya Ibungilo na timu ya kata ya Shibula na
fainali yake kufanyika siku ya jumatatu Septemba 17, 2018 katika uwanja
wa CCM Kirumba mgeni rasmi akiwa Naibu Waziri wa Sera, Bunge Kazi
,Ajira, Vijana na Walemavu Mhe Antony Mavunde.
‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’
Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
14.09.2018.







No comments:
Post a Comment