WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuimarisha kilimo cha
mbegu za mafuta iliTanzania iachane na uagizaji wa mafuta ya kula
kutoka nje.
Amesema
malengo ya kampeni hiyo ni kuhakikisha kuwa mkoa wa Kigoma na maeneo
mengine yenye fursa ya kulima zao la chikichi yanaimarisha kilimo hicho.
“Hivi sasa, nchi yetu inatumia takribani Dola za Marekani milioni 294
kila mwaka kwa ajili ya kuagiza mafuta hayo.”
Ametoa
kauli hiyo jana (Ijumaa, Septemba 14, 2018) katika hotuba yake
aliyoitoa wakati wa kuahirisha Mkutano wa 12 wa Bunge jijini Dodoma.
Bunge limeahirishwa hadi Novemba 6, mwaka huu.
Amesema
sambamba na azma ya Serikali ya kuweka mkazo katika kusimamia
uzalishaji na masoko ya mazao makuu matano ya biashara ambayo ni pamba,
kahawa, korosho, chai na tumbaku, Serikali imedhamiria pia kupanua wigo
kwenye mazao mengine muhimu ikiwemo chikichi, alizeti na ufuta ili
kukidhi uzalishaji wa mbegu za mafuta nchini.
“Katika
kutekeleza azma ya Serikali, kuhusu kuongeza uzalishaji wa mafuta ya
kula nchini, tarehe 28 Agosti, 2018 nikiwa mkoani Kigoma nilizindua
kampeni maalumu ya kuendeleza zao la chikichi ambalo kwa sasa
linatambulika kama zao kuu la sita la kipaumbele,” amesema.
Amesema
ili kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa mahitaji ya mafuta ya kula,
Serikali imeweka mikakati ya kuendeleza zao la chikichi kwa kuanzisha
kituo cha utafiti wa zao la chikichi katika eneo la Kihinga, mkoani
Kigoma.
“Serikali
imeandaa mpango mkakati wa uzalishaji wa miche bora ya chikichi milioni
20 ifikapo mwaka 2021. Kwa kuanzia, mwaka 2018/2019, Serikali
inakusudia kuzalisha miche bora ya chikichi milioni 10 ambayo
itasambazwa kwa wakulima,” amesema.
Aidha,
Waziri Mkuu amesema Serikali pia imeandaa mpango mkakati wa miaka
mitano wa utafiti wa mbegu bora ili kuongeza tija kutoka tani 1.6 hadi
kufikia tani 4.0 za matunda ya chikichi kwa hekta kwa mwaka.
Amesema
Serikali imeweka mazingira mazuri ya kuvutia uwekezaji na matumizi ya
teknolojia ya kisasa kwa ajili ya uchakataji zao la chikichi na imepanga
kusimamia vituo vikuu vya uzalishaji vya gereza la Kwitanga, Ilagala na
JKT Bulombora.
Amewataka
Watanzania wachangamkie fursa ya kilimo cha zao la chikichi ili nchi
iweze kujitosheleza kwa mafuta ya kula na ziada kuuza nje. “Nitoe rai
pia kwa wawekezaji, waje kuanzisha viwanda vya kuchakata chikichi na
mazao yake,” amesisitiza.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali kwa upande wake,
inaimarisha taratibu za uingizaji wa sukari na mafuta ya kula kwa kuweka
madaraja na usimamizi makini.
Ameitaka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo wakamilisha jukumu hilo kwa wakati.
“Pia,
naagiza vyombo vya dola viongeze ushirikiano na mamlaka husika ambazo
ni TRA, TFDA, Bodi ya Sukari na TBS ili kudhibiti uingizaji holela wa
sukari na mafuta ya kula ikiwa ni pamoja na kuziba mianya ya magendo,”
amesema.

No comments:
Post a Comment