Tuesday, September 18, 2018

MHE MAVUNDE AHITIMISHA MASHINDANO YA ANGELINE JIMBO CUP 2018.

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mku, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Mhe Anthony Mavunde amefunga mashindano ya Angeline Jimbo Cup 2018 kwa kukabidhi Kitita cha shilingi milioni mbili na laki moja, Jezi seti moja, mpira mmoja na kikombe kimoja  kwa Timu ya Kata ya Ibungilo mara baada ya kuibuka mshindi wa mashindano hayo kwa kuifunga Timu ya Kata ya Kirumba kwa mikwaju ya penati  baada ya kutoka sare ya kufungana goli moja kwa moja baada ya dakika 90 za mchezo.

 Akizungumza kabla ya kukabidhi zawadi hizo, Mhe Mavunde amempongeza Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula kwa uamuzi wake wa kuanzisha mashindano hayo yenye lengo la kuibua na kukuza vipaji vya michezo ndani ya Jimbo lake huku akiziasa timu pinzani kukubaliana na matokeo na kujipanga upya kwa mashindano hayo awamu ijayo

‘… Kama nilivyokuwa nmeanza kusema timu iliyojiandaa vizuri itashinda na kweli Ibungilo imeshinda, Kirumba wanajua mpira lakini tukubali  Ibungilo wanajua zaidi …’ Alisema

Aidha ameongeza kuwa michezo ni sehemu ya furaha, sehemu ya kujenga umoja na mshikamano hivyo kuwataka wananchi na wachezaji wa mashindano hayo kuendeleza upendo na mshikamano walionao.

Kwa upande wake afisa Michezo wa manispaa ya Ilemela Ndugu Kizito Bahati mbali na kuelezea historia fupi ya mashindano hayo, ametaja mafanikio yaliyopatikana kupitia mchezo huo ikiwemo kuibua vipaji vipya na kuviendeleza vile vya awali huku akitolea mfano wa mashindano ya mwaka 2016 ambapo baadhi ya wachezaji walisajiliwa na timu za ligi kuu na za daraja la kwanza na wengine wakifanikiwa kuingia timu ya taifa (Serengeti Boys) akiwemo mchezaji Cyprian Benedictor, Kelvin Prosper na Ally Ally  kisha baadae kuhamia Mbao Fc na KMC ya Jijini Dar es Salaam.

Nae Nahodha wa Timu ya Ibungilo Damian Paul mbali na kuelezea ugumu wa mchezo dhidi ya Timu ya Kata ya Kirumba,  amewasifu wapinzani wao kwa kucheza mpira mzuri katika kipindi cha kwanza na cha pili mpaka kufanikiwa kusawazisha goli walilokuwa wamefungwa huku akisisitiza kuwa Timu yake kuifunga Timu pinzani si jambo geni kwani hata katika mechi ya ufunguzi walikutana na walifanikiwa kuifunga.

Akihitimisha, Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula amewashukuru wadau alioshirikiana nao katika kufanikisha mashindano hayo sambamba na kuwaomba wadau wengine kujitokeza kumuunga mkono ili kufanikisha tena mashindano hayo kwa awamu ijayo.

Katika mashindano hayo, Timu ya Kata ya Kirumba ilifanikiwa kushika nafasi ya pili na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Mhe Kheri Denice James kuikabidhiwa kitita cha shilingi milioni moja na laki sita, jezi seti moja, mpira mmoja  na kikombe huku Timu ya Kata ya Shibula ikishika nafasi ya Tatu na Mkuu wa Mkoa Simiyu Mhe Antony Mtaka kuikabidhi kitita cha shilingi milioni moja, jezi seti moja, mpira mmoja na kikombe, Wakati Mbunge wa Jimbo la Nyamagana Mhe Stanslaus Mabula akikabidhi zawadi kwa waandishi bora wa mashindano hayo, Upande wa TV akiwa ni Edmund Rutta kutoka BarmedasTv, Gazeti akiwa Sheila Katikula kutoka Mtanzania na Redio akiwa Maridhia Ngemela wa City Fm  waliojinyakulia laki moja kila mmoja.

‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’


Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela











No comments:

Post a Comment