IKIWA
msimu wa kununua mazao umeanza, Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Vumilia Zikankuba amewataka
wakulima kuhakikisha wanazingatia ubora wa mahindi.
Aidha,
amesema nchi inachakula cha kutosha na kusisitiza kuwa katika msimu wa
kwanza wa ununuzi wa mahindi bei ya NFRA ni wastani wa Sh 380 hadi Sh
400 kwa kilo.
Akizungumza
na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Dodoma, Zikankuba alisema
NFRA haitaweza kununua mahindi mabovu na kusisitiza wakulima kuwa na
mahindi yenye ubora ambayo yatawasaidia kupata masoko ya nje pia.
"
Haiwezekani NFRA itumia fedha za Serikali kununua mahindi yasiyokidhi
viwango vya ubora na machafu kutoka kwa wakulima. Hivyo wakulima
wanapaswa kuzalisha mahindi kwa kuzingatia viwango vya ubora
vinavyokidhi vigezo vya soko..
Aliongeza:
“Lazima chakula tunachonunua kizingatie ubora. Tunataka tubadilishe
taswira ya NFRA kwa sababu awali kulikuwa na tatizo la chakula
kuharibika kwa kipindi kifupi.”
Zikankuba
alisema ili kuhakikisha mahindi ya wakulima yanaweza kukidhi viwango
vinavyotakiwa NFRA tayari imekwishatoa elimu kwa wakulima kupitia
vikundi na kwenye vyombo vya habari.
Alibainisha
kuwa baada ya elimu hiyo wakala umefanikiwa ambapo wakulima kutoka
maeneo ya Makambako, Sumbawanga na Mpanda wameanza kuzalisha na kuuza
mahindi yenye ubora kwa NFRA.
“Changamoto
iliyopo ni kwa baadhi ya wakulima wachache ambao bado wamekuwa wagumu
kubadilika na wale ambao wanaamini wakitumia nafasi zao wanaweza kuuza
mahindi yasiyo na ubora,"
Alisema
kwa mkulima kuwa na mahindi yenye ubora unatoakiwa utasaidia katika
kupata soko la NFRA, pia katika taasisi zingine zinazonunua nafaka hiyo
za ndani na nje ya nchi.
"Dhima
ya serikali ni kwenda uchumi wa kati kupitia uchumi wa viwanda, kwa
mahindi pekee hayatumiki kwa chakula pekee, bali kutengeneza bidhaa
mbalimbali. Hivyo hatuwezi kufikia Tanzania ya viwanda endapo wakulima
watazalisha malighafi zisizokuwa na ubora,” alieleza.
Viwango
vinavyopaswa kuzingatiwa na wakulima wa mahindi ni kwamba unyevunyevu
usizidi asilimia 13.5, takataka asilimia 0.5 na punje zilizovunjika
zisizidi kwa asilimia 2.
Viwango
vingine ni punje zilizoliwa na wadudu na zilizosinyaa zisizidi asilimia
moja, punje mbovu asilimia mbili na punje za rangi tofauti zisizidi
asilimia 0.5.
Zikankuba alitoa msisitizo kwa wakulima kutunza chakula badala ya kukiuza chote.
“Msimamo
wa Rais (John Maguful) wa kutotoa chakula cha msaada upo sahihi kwa
sababu kuna maeneo walikwishazoea kupelekewa chakula cha msaada. Msimamo
huo umelenga kuwahamasisha wananchi kutunza chakula, haya malalamiko ya
hatuna chakula yanachangiwa na uzembe wa wananchi wa kuuza chakula
chote,” Vumilia, alibainisha.
Alisema
jukumu la wakala ni kutunza chakula kwa ajili ya dharura kama kumetokea
majanga kama mafuriko, njaa, tetemeko na majanga mengine ambayo
wanachi watahitaji msaada wa chakula.
Kuhusu
bei ya mahindi ambayo NFRA imeanza kununua mahindi kwa wakulima
Zikankuba alisema ni wastani wa Sh 380 kwa kilo hadi Sh 400 kwa kilo
kulingana na eneo na eneo, na ni bei inayoendana na mwenendo wa bei ya
soko.
“
Mfano bei ya soko ya mahindi mkoani Ruvuma ni Sh 250 kwa kilo, lakini
sisi kama NFRA tunanunua kwa bei ya juu ya kuanzia Sh 350 hadi 380 kwa
kilo," alisema.
Aliongeza:
“Mkoani Dodoma NFRA inanunua Sh 420 kwa kilo, Makambako Sh 400,
Shinyanga Sh 500, Katavi na Ruvuma Sh 350 hadi 380. Bei hiyo bado ni ya
juu ukilinganisha na bei ya soko iliyopo,” alifafanua.
Aidha,
Zikankuba alisema ziada ya mazao yote yaliyozalishwa na wakulima msimu
huu imefikia tani milioni 2 huku ziada ya mahindi pekee ni tani 970,000.
Zikankuba
alisema NFRA imetengewa Sh bilioni 15 kwa ajili ya kununua tani 28,000
kwa awamu ya kwanza ikiwa ni asilimia 2 ya ziada ya mahindi iliyopo.
Zikankuba
alisisitiza kuwa NFRA inazingatia ubora wakati wa kununua kwa kuwa ni
haki na muhitaji kupatiwa chakula bora na Salama kwa afya wakati wa
dharula hivyo mahindi ambayo hayana ubora yakituzwa kwa muda mrefu
ghalani yanakuwa na nafasi kubwa kupata vimelea vya fangasi ambao
husababisha uwepo wa sumu kuvu katika nafaka hiyo.
Alisema
kuwa Sumu kuvu ni hatari sana kwa afya ya mlaji. Tatizo hili kwa kiasi
kikubwa sana, linaweza kuepukika kwa mkulima kufuata mbinu bora za
kilimo, mbinu bora za utayarishaji nafaka na mbinu bora za kuhifadhi
nafaka baada ya kuvuna. Lengo la NFRA ni kutoa chakula chenye ubora na
salama wakati wa dharula.
MWISHO

No comments:
Post a Comment