Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema ni ruksa kwa wakulima kuuza mahindi nje ya nchi ilimradi watoe taarifa serikalini.
Katika
majibu yake kwa maswali ya papo kwa hapo bungeni leo Alhamisi Novemba
8, 2018, Waziri Mkuu amesema pia Tanzania inaruhusu kuingiza mahindi
ndani ya nchi ilimradi kuwepo na vibali maalumu kutoka katika mamlaka
husika.
Katika
swali lake, Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Lucy Mlowe ametaka kujua
nini kauli ya Serikali kuhusu mahindi mengi ambayo yamekosa soko na
kuwakosesha kipato wakulima ikiwemo mkoa wa Rukwa.
"Wakulima
wanaruhusiwa kuuza mahindi nje ya nchi, jambo la muhimu hapa ni
kuhakikisha kunakuwepo na taarifa sahihi ndani ya Serikali ili tuweze
kujiridhisha kama nchi ina chakula cha kutosha," amesema Waziri Mkuu.
Katika hatua nyingine, Majaliwa amekiri kuwepo kwa viwanda vichache vya mbolea kunasababisha bei ya mbolea kupanda zaidi.
Amesema
Serikali imeiona changamoto hiyo na imeshazungumza na wawekezaji kutoka
Ujerumani ambao watajenga viwanda Kilwa na Mtwara ambapo vitaungana na
kiwanda cha Minjingu na mbolea itazalishwa kwa wingi na kupunguza bei.
Majaliwa
alikuwa akijibu swali la Neema Mgaya (Viti Maalum-CCM) aliyetaka kujua
nini mkakati wa Serikali kuongeza uzalishaji wa mbolea ambapo asilimia
90 inatoka nje.

No comments:
Post a Comment