Sunday, June 9, 2019

AFISA ELIMU ILEMELA AFUNGA RASMI MASHINDANO UMITASHUMTA NGAZI YA WILAYA.

Afisa Elimu Msingi wa Manispaa ya Ilemela ndugu Marco Busungu amefunga rasmi mashindano ya UMITASHUMTA yaliyofanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari Bwiru Wavulana  June 06, 2019 yakikutanisha zaidi ya wanafunzi 400 kutoka shule za msingi za wilaya hiyo.

Akifunga mashindano hayo, Afisa elimu huyo amewaasa waratibu wa mashindano hayo kuhakikisha wanakuwa waadirifu kwa kupendekeza wachezaji wenye uwezo  watakaounda timu ya wilaya kushiriki ngazi ya mkoa ili kurudi na ushindi kwa wilaya yao na kupata fursa ya kuingia katika timu ya mkoa kushiriki ngazi ya taifa, Michezo ambayo itachezwa mkoani Mtwara kitaifa.

Kwa mwaka huu 2019, mashindano ya UMITASHUMTA yamehusisha mchezo wa mpira wa miguu , pete, kikapu, mikono, wavu, riadha na sanaa za maonesho na timu za shule za msingi zikiungana pamoja kwa kutengeneza kanda nne, kanda ya Bugogwa, Buswelu, Bwiru na Pasiansi zikishindanishwa.


Aidha Mwalimu Busungu ameipongeza kanda ya Bugogwa kwa kuwa kinara wa mashindano hayo kwa mara ya tatu mfululizo huku akizitaka kanda nyengine kuongeza jitihada  na kufanya vizuri.


Akisoma taarifa ya mashindano hayo afisa michezo manispaa ya Ilemela Kizito Bahati amesema kuwa baada ya zoezi la ufungaji wa mashindano hayo jumla ya wanafunzi 100 watachaguliwa kuunda timu ya wilaya itakayoshiriki ngazi ya mkoa wakiambatana na walimu 16 na daktari mmoja, huku mashindano hayo ya ngazi ya mkoa yakitarajiwa kuanza mapema hivi karibu katika viwanja vile vile vya shule ya wavulana Bwiru.












No comments:

Post a Comment