Wananchi wa Jimbo la Ilemela wameaswa kuhakikisha wanajiunga na Bima ya Afya iliyoboreshwa ili kuwa na uhakika wa matibabu pindi wanapopatwa na magonjwa ikiwemo yale ya dharula.
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Kirumba katika viwanja vya Shule ya msingi Bugungumuki ambapo amewataka wananchi hao kuona haja ya kujiunga na Bima ya Afya iliyoboreshwa (Community Health Fund) inayopatikana kwa gharama nafuu ya shilingi elfu 30,000/= kwa Kaya yenye idadi ya watu 6 ambapo wataweza kutibiwa bure katika Zahanati, Kituo cha Afya, Hospitali ya wilaya hadi ya mkoa pale ugonjwa wa mnufaika na Bima hii utakuwa haujapata tiba sahihi kwa ngazi za chini, kwa kipindi cha mwaka mzima
'.. Hakuna mwenye garantii na Mungu, Hatujui lini na muda gani utaugua na mbaya zaidi je wakati unaugua utakuwa na fedha za matibabu??, Lakinii hapa unatoa elfu30 tu utatibiwa wewe, mwenza wako na wengine wanne kufikisha idadi ya watu 6 ..' Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula amewaasa vijana wa Jimbo hilo kutumia fursa za kujikwamua kiuchumi zinazojitokeza, pamoja na kuacha kuchagua kazi kwani wengi wamekuwa hawajitokezi kuchukua mikopo inayotolewa na manispaa, Na wachache wanaojitokeza wamekuwa sio waadirifu pamoja jitihada kubwa zilizofanywa na Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli za kuondoa riba katika mikopo hiyo.
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo Mhe Alex Ngusa mbali na kumshukuru mbunge huyo na Rais Mhe Dkt John Magufuli kwa miradi mikubwa ya kimaendeleo inayotekelezwa katika kata yake amelalamikia watumishi wa afya wasiokuwa waadirifu, wanaotoa lugha chafu na manyanyaso kwa wagonjwa pindi wanapofata huduma, Jambo ambalo Mhe Mbunge ameshalichukulia hatua.
Nae afisa Ardhi na Mipango miji wa manispaa ya Ilemela Ndugu Shukran Kyando amekemea vitendo vya kitapeli na viovu vinavyofanywa na baadhi ya wananchi vya kuuza maeneo yaliyokwisha fidiwa, Jambo linaloongeza migogoro ya ardhi isiyo ya lazima na vitendo vya kutokulipa Kodi ya ardhi kwa wakati vinavyochangia kurudisha uchumi nyuma.
Mkutano huu wa kawaida wa kusikiliza kero za wananchi ulihudhuriwa pia na mwenyekiti wa UVCCM Taifa Comred Kheri James mkaazi wa Kirumba, Katibu wa CCM wilaya ya Ilemela, wataalamu wa manispaa, Diwani wa kata ya jirani ya Kawekamo, Mkuu wa polisi wilaya ya Ilemela na viongozi wengine kutoka ngazi ya kata.
' Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga'
Imetolewa na
Ofisi ya mbunge
Jimbo la Ilemela
June 08, 2019.








No comments:
Post a Comment