Walimu na viongozi wa kamati za shule wametakiwa kutowarudisha watoto nyumbani na katisha masomo kwa makosa ya wazazi kushindwa kuchanga michango wanayokubaliana katika jamii kwaajili ya kuboresha miundombinu ya kujifunzia na kufundishia.
Agizo hilo limetolewa na Afisa Tarafa wa wilaya ya Ilemela, Ndugu Godfrey Mzava wakati akizungumza na wananchi wa kata ya Nyamhongolo katika viwanja vya shule ya msingi Nyamhongolo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kuzipatia ufumbuzi ambapo amekemea vitendo vinavyofanywa na baadhi ya walimu na viongozi wa kamati za shule vya kuwakatisha wanafunzi masomo baada ya wazazi wao kushindwa kutekeleza makubaliano wanayoafikiana katika vikao vya kuchangia shughuli za maendeleo pamoja na kutumia vibaya fedha za miradi ya maendeleo kwa maslahi binafsi
‘.. Kuanzia leo ni marufuku kumrudisha mtoto nyumbani eti kwa sababu mzazi wake hajachangia mchango wowote ule shuleni, Kama mlikubaliana wenyewe kwenye vikao vyenu basi shikaneni wenyewe lakini sio mtoto, Kufanya hivyo ni kumdhurumu haki yake ya msingi ya kusoma na tunakuwa hatujafanya sawa ..’ Alisema
Aidha Gavana Mzava amekemea vitendo vya uvamizi wa maeneo ya Umma hasa yale ya taasisi kama shule sanjari na kumuagiza afisa elimu wa kata hiyo Bwana Erasto Fred kuusimamisha Uongozi wa kamati ya shule hiyo, Kufuatia kulalamikiwa na wananchi huku akiwaomba kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya tano chini ya Mhe Rais Dkt John Magufuli katika kuboresha sekta ya Elimu na utoaji wa elimu bila malipo.
Akimkaribisha Gavana Mzava, Diwani wa kata ya Nyamhongolo … amemshukuru kwa kuizuru kata yake, Pamoja na kumuahidi ushirikiano katika kumaliza kero na changamoto za wananchi huku akibainisha hatua mbalimbali zilizochukuliwa na kamati yake ya maendeleo ya kata katika kumaliza kero zinazohusu uongozi wa shule ya msingi Nyamhongolo ikiwemo kukamata wezi walioiba mifuko ya saruji iliyokuwa ikitumika katika ujenzi wa madarsa mapya ya shule na kuwafikisha katika vyombo vya dora kwa hatua zaidi za kisheria.
Kikao hicho cha kusikiliza kero za wananchi kata ya Nyamhongolo, kilihudhuriwa pia na diwani wa viti maalumu kutoka kata ya Nyamhongolo Mhe Safia Mkama, wataalamu wote wa ngazi ya kata, wenyeviti wa mitaa 12 ya kata hiyo na wazee wanaoishi eneo hilo.








No comments:
Post a Comment