Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi na Viongozi wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kutangaza mazuri yanayofanywa na Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Daktari John Magufuli kwa wananchi kama ishara ya kuunga mkono juhudi hizo za kuwaletea maendeleo.
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Mwanza Mhe Kemilembe Lwota wakati akifungua kikao cha Baraza la Umoja wa Wanawake (UWT) wilaya ya Misungi ambapo amewataka kuunga mkono juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Mhe John Magufuli za kujenga miundombinu ya barabara, reli ya kisasa, upanuzi wa uwanja wa ndege, ununuzi wa ndege mpya, ukarabati wa vyombo vya majini,utoaji wa elimu bure na uboreshaji wa huduma za afya kwa kujenga vituo, zahanati na hospitali mpya za wilaya nchi nzima
‘.. Tusiogope kuyasema mazuri yanayofanywa na Rais wetu mpendwa, Ameturahisishia kazi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa na huu mkubwa unaokuja, Kiongozi wetu amefanya mengi makubwa nyie wenyewe ni mashahidi kazi yetu ni kuyasema haya mazuri kwa wananchi wenzetu ili wajue nini Serikali yao imefanya ..’ Alisema
Aidha Mhe Lwota amewaasa wanawake wote nchini kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali za Uongozi katika uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni na kuwaunga mkono wanawake wote watakaojitokeza kugombea nafasi hizo bila kujali tofauti walizonazo huku akiwakumbusha kushiriki zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake (UWT) Wilaya ya Misungwi, Bi Bahati Makala amemshukuru Mbunge huyo kwa ugawaji wa Sare za Wanawake wa UWT, Kukubali kushiriki pamoja nao katika shughuli za kuimarisha chama na jumuiya hiyo huku akimuahidi ushirikiano katika kuhakikisha chama kinaimarika na kuisaidia Serikali katika kutekeleza shughuli za kimaendeleo.
Shughuli hiyo pia ilihudhuriwa na Kaimu katibu wa UWT Mkoa wa Mwanza Bi Salama Muhampi, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mwanza Comrade Lufungulo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Mhe Antony Bahebe.





No comments:
Post a Comment