Thursday, April 21, 2022

DKT MABULA AKABIDHI SADAKA YA FUTARI KWA TAASISI ZA ELIMU JIMBO LA ILEMELA

 Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula Leo amekabidhi sadaka ya futari Kwa  taasisi za Elimu zilizopo ndani ya Jimbo hilo ikiwemo shule ya sekondari Bwiru wavulana, Chuo Cha Mipango na shule ya sekondari Bwiru wasichana ambapo Sukari Kilo 110 zilitolewa Kwa kila taasisi, Mchele Kilo 110 kwa Kila taasisi, Tambi na Tende Ili wanafunzi waislamu waweze kupata futari katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan


Akizungumza wakati wa makabidhiano ya sadaka hiyo, Katibu wa Mbunge Ndugu Kazungu Safari Idebe amesema kuwa Mbunge wa Jimbo la Ilemela amekuwa na utaratibu wa kuungana na waumini wa dini ya kiislamu kila mwaka unapofika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa kutoa sadaka ya futari ili kusaidia waumini hao waweze kufunga kwa salama na amani 

'.. Mhe Mbunge alitamani kuwepo yeye mwenyewe katika zoezi hili, Lakini kutokana na majukumu ya kitaifa aliyopewa ameshindwa ingawa siku za hivi karibu alianzisha yeye mwenyewe zoezi hili Kwa kutoa sadaka hii katika vituo vya watoto yatima, Wajane, Misikiti, Wazee na Watu wenye uhitaji, Na leo sisi wasaidizi wake akaamua tumuwakilishe kuendelea alipoishia..' Alisema

Aidha Ndugu Kazungu amefafanua kuwa Serikali na nchi Kwa ujumla  ina mategemeo makubwa Kwa wanafunzi hao na kuwaasa kuutumia mwezi huu mtukufu kuombea taifa na viongozi wake wakiongozwa na Rais Mhe Samia Suluhu Hassan sanjari na kuongeza kuwa taifa lolote lenye hofu ya Mungu lazima liwe na Maendeleo 

Kwa upande wake Mkuu wa shule ya sekondari Bwiru wasichana Mwalimu Mektilda Shija mbali na kumshukuru Mbunge huyo amesema kuwa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Mabula amekuwa mtu wa msaada katika shule yake na si mara ya kwanza kufika kutoa misaada kwani mara kadhaa amekuwa akishirikiana nao katika kutatua kero mbalimbali zinazoikabili shule hiyo hivyo kuwataka wanafunzi wake kumuombea hasa katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan

Hawa Japhari ni mwanafunzi wa kidato Cha Tano anaesoma masomo ya mchepuo wa sayansi (CBG) katika shule ya wasichana Bwiru amempongeza na kumshukuru Mbunge Mhe  Dkt Angeline Mabula Kwa msaada alioutoa pamoja na kumuombea Kwa Mungu Ili kidogo alichokitoa aweze kuzidishiwa





No comments:

Post a Comment